TaarifaNews Team
Wakaazi wa Nyando kule Kisumu walivamia nyumbani kwa mwanaume mmoja ambaye anakisiwa kuhusika katika mauji ya mwanamke kwa jina Molly ambaye amekuwa naye kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Wakaazi waliojawa na gadhabu asubuhi ya leo walivunja nyumba ya mfanyabiashara huyo na kuwasha moto kwenye gari lake kwa madai kuwa alihusika na kifo cha mwanamke huyo.
Inadaiwa kwamba mshukiwa alimpeleka mwanamke huyo kwa likizo, wiki moja iliyopita huko Migori, ambapo mwili wake ulipatikana eneo la Awendo, Kaunti ya Migori.
Akizungumza na Radio Moja nchini, Mary Akinyi Amollo anasema kuwa marehemu alimtumia ujumbe mfupi dada yake mara tatu kwamba maisha yake yalikuwa hatarini kwenye mikono ya mtu ambaye alikuwa naye kutoka Mei 3.Baadaye simu yake ilizimwa.
“Marehemu anajulikana kwa jina la Molly kutoka Ayweyo huko Nyando. Waliondoka na mpenzi wake kwa likizo huko Migori. Siku chache baadaye msichana alimtumia dada yake ujumbe kuwa alikuwa katika hatari. Ujumbe huu ulitumwa mara nne,” alisema Mary.
“Jana ilitangazwa kwamba mwili usiojulikana umepatikana katika mto Awendo huko Migori. Leo asubuhi familia yake ilikwenda kwenye chumba cha maiti na kugundua kuwa alikuwa binti yao,” aliongeza.
Tukio hilo liliwakasirisha wanafamilia wa aliyefariki ambao walilazimikakuchukua sheria mikononi mwao.
“Leo mwendo wa saa Kumi alfajiri, wanafamilia waliokasirika walivamia klabu Moja pale Ahero ambapo mtuhumiwa anayefanya kazi kama meneja na kuteketeza gari lake la saloon na kuendelea mbale na kuharibu moja ya nyumba yake ya upangishaji katika eneo hilo,” akaongeza.
Mshukiwa huyo pamoja na wake zake watatu walikimbilia kituo cha Polisi cha Ahero kwa usalama wao.
Mwili wa marehemu sasa uko katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Ombo huko Migori ukisubiri uchunguzi wa mwili.