Baadhi ya Wakilishi wodi kaunti ya Nairobi sasa wametaja hatua ya serikali ya kaunti ya Nairobi kuita barabara ya Dikdik kule Kileleleshwa kuwa jina la katibu mkuu wa muungano wa COTU Francis Atwoli kama utovu wa sheria.
Mwenyekiti wa kamati inayohusika kufanikisha shughuli za bunge ambaye ni MCA wa Karen David Mberia ameshtumu kaimu gavana Ann Kananu kwa kuharikisha swala hilo bila kufuata sheria.
Kulingana na Mberia haijapita siku sitini tangu hoja hiyo iletwe bungeni na kwamba siku za kuifanikisha haikuwa imefika.
‘‘Nimepata mshangao mkubwa mimi kama mwenyekiti wa kamati ya utekelezwaji wa maswala ya bunge barabara hii ya Atwoli kwani hoja yenyewe haijafika katika kamati yetu ipo bado bungeni na si sheria kuitekeleza kwa sasa,jameni sijui ni siku gani Kananu na serikali ya kaunti itaheshimu bunge hili na kufanya vitu kwa mujibu wa sheria.’’ Mberia alisema.
Ameshtumu pia serikali ya kaunti kwa kutofanikisha hoja za mashujaa kama vile Joe Kadenge ambapo kuna barabara kule South B ambayo inafaa kuitwa mwanasoka huyo mkongwe lakini mpaka sasa hayo yamemwagiliwa maji.
‘‘Kuna barabara ambayo tulipitisha hoja bungeni ya Joe Kadenge mpaka sasa hawajafanya hivyo..kama kamati tumezungumza na mhandisi Ochieng kuhusu swala hili lakini bado hajatupa jibu.’’ Aliongeza
Atwoli ametaja hatua hiyo kama furaha kwake kwani ametetaa wafanyikazi dunia nzima.