• Sun. May 19th, 2024

Jaribio la Kujitoa Uhai Latibuka Baada ya Mshukiwa Kumuua Mkewe

Oct 6, 2021
291 300

Huku visa vya kujitoa uhai vikiendelea kukithiri haswa kati ya wapenzi waliotonesha doa kwenye ndoa au penzi lao, mwanamume mmoja anazuiliwa na polisi Nakuru baada ya kumwua mkewe kabla ya kujaribu kujitoa uhai kwa kuruka kutoka kwenye ghorofa ya nne.

Paul Ochieng anayefanya kazi katika kampuni moja ya kutengeneza nishati ya mvuke, anadaiwa kumwua kwa kumdunga kisu mkewe, 25, kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Wapangaji wa Stadium Flats Nakuru waliokatizwa kwenye shughuli zao za maandalizi ya chajio na mkasa huo wa hapo jana, walibaki vinywa wazi walipokumbana na mwili wa jirani yao aliyedungwa kisu cha moyo na kufa papo hapo.

Akihofia ghadhabu ya umma uliopandishwa mori na unyama wake, Ochieng alinyatia pembeni mwa chumba chao na kujirusha chini akikusudia kujitoa uhai.

Hata hivyo, jaribio hilo liligonga mwamba kwani alipata majeraha mabaya miguuni tu.

Majirani wenye butwaa walipiga ripoti kwa polisi kupitia chumba cha mawasiliano cha kituo cha Bondeni, ambapo maafisa wa polisi akiwemo kamanda wa polisi Nakuru walifika kwenye eneo la tukio kwa upesi.

Taarifa za mkasa huo zilirekodiwa huku kisu kilichotumika kwa mauaji kikihifadhiwa ili kutumika kama ushahidi, baada ya mshukiwa aliyenusurika kifo kufikishwa mahakamani.

Kwa sasa, mshukiwa anatibiwa kwenye hospitali ya PGH Nakuru chini ya ulinzi wa polisi akisubiri kufunguliwa Mashtaka ya mauaji pamoja na yale ya kujaribu kujitoa uhai, huku mwili wa mwendazake ukihifadhiwa kwenye makafani ya hospitali ya Jack kabla ya kufanyiwa upasuaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *