• Mon. May 6th, 2024

Amri Kali yatolewa kwa Raila, Ruto

Jul 19, 2023
197 300

Shinikizo zimetolewa kwa Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga kulegeza misimamo yao mikali na kuzungumza ili kutatua mzozo unaokumba nchi na kuepusha maandamano ambayo yamesababisha vifo na uharibifu wa mali.

Mabalozi wa nchi 13 za kigeni wakiwemo wa Amerika na Uingereza, sasa wanahimiza viongozi hao wawili kuketi na kuzungumza ili kuepusha vifo vinavyotokea katika maandamano yanayoitishwa na Upinzani.

Azimio imeshikilia kuwa maandamano yataendelea leo Jumatano, kesho Alhamisi na Ijumaa jinsi ilivyopangwa ili kushinikiza serikali kupunguzia raia gharama ya maisha.

“Tunahuzunishwa na vifo, na tuna hofu kuhusiana na viwango vya juu vya ghasia ikiwemo matumizi ya risasi na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya hivi majuzi,” mabalozi hao walisema kwenye taarifa ya pamoja.

Mabalozi wa Australia, Canada, Ujerumani, Denmark, Uholanzi, Uswizi, Ireland, Norway na Ukraine walitia saini taarifa hiyo.

Huku wakikiri kwamba hali ya maisha imekuwa ngumu kwa Wakenya wengi, mabalozi hao walihimiza viongozi kuzika tofauti zao kwa ajili ya amani na kujenga nchi yao kwa ushirikiano.

Mabalozi hao wametoa onyo hilo siku chache baada ya Afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu kukashifu ghasia na maafaa yaliyoshuhudiwa katika maandamano ya Jumatano wiki jana.

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake Jeremy Laurence, shirika hilo lililaani maafisa wa polisi waliotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na hivyo kusababisha mauaji.

“Tunataka uchunguzi wa haraka na huru ufanywe kuhusu vifo na majeraha yaliyotokea katika maandamano hayo. Waliohusika na mauaji hayo sharti wachukuliwe hatua za kisheria. Na serikali iweke mikakati ya kuzuia vifo na maafa katika siku zijazo,” akasema Bw Laurence. Nalo shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Hazina ya Watoto (UNICEF) mnamo Ijumaa wiki jana lilisema watoto wanafaa kulindwa nyakati za maandamano ya kupinga serikali. Wakati huo huo, Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kimeitisha Mazungumzo ya Kitaifa ya kujadili changamoto zinazochochea maandamano.

Read Also:Ubongo yatimiza Miaka 10 Katika Burudani ya Elimu

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana Jumanne, Rais wa chama hicho, Eric Theuri alipendekeza kuwa mazungumzo hayo yashirikishe wanasiasa, viongozi wa kidini, wanasheria, makundi ya kijamii pamoja na wadau wengine.

“Tunaitisha mazungumzo jumuishi baada ya kung’amua kuwa mazungumzo yaliyoendeshwa na wabunge pekee yalifeli kutoa mwelekeo wa kusuluhisha shida zinazokumba taifa hili. Hii ndiyo maana tunataka mazungumzo yanayoshirikisha wadau wengine wote mbali na wanasiasa,” akaeleza.

Licha ya wito wa mabalozi na mashirika ya haki za binadamu ya kimataifa, Rais William Ruto ameapa kuwa hatazungumza na Bw Odinga huku muungano wa Azimio ukisema hauwezi kufanya kazi na serikali ukidai ni haramu. Katika taarifa ya kusisitiza msimamo wa Rais, Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki jana Jumanne alionya kuwa polisi wameagizwa kuwakabili vikali watakaozua ghasia katika maandamano ya leo, kesho na Ijumaa ambayo alidai serikali ilifahamu kupitia vyombo vya habari.

“Wanaopanga kuzua ghasia na kuharibu mali leo, Alhamisi na Ijumaa mtakabiliwa vikali na nguvu kamili za maafisa wa usalama,” Bw Kindiki aliapa.

Upinzani, kwa upande wake, unasema kwamba maandamano yao yanalenga kushinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha inayokumba Wakenya kupitia Sheria ya Fedha ya 2023.

Vinara wa Azimio katika kikao na wanahabari mnamo Jumanne, waliilaumu serikali kwa kuwatishia maisha kwa wito wao wa maandamano ambayo walisisitiza yataendelea licha ya onyo kali la serikali.

Walisema serikali imewapokonya walinzi viongozi wote wa Upinzani wanaounga maandamano.

“Hata wakitutisha na kuondoa walinzi wetu, Azimio inathibitisha kwamba maandamano yaliyopangwa Jumatano (leo), Alhamisi na Ijumaa wiki hii yatafanyika,” vinara wa muungano huo walisema kwenye taarifa.

Walisema kwamba wana habari kuwa serikali inatumia kikosi spesheli (OSU) kuwalenga na kuwaua waandamanaji na wakaapa kutotishika wakisisitiza kuwa wamekuwa wakihimiza wafuasi wao kudumisha amani.

Walirejelea kauli ya Rais Ruto kwamba “atasafirisha” Bw Odinga na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakisema wana habari anapanga kutumia kikosi hicho cha OSU kuwadhuru viongozi wa Upinzani.

“Makosa yetu ni kutaka serikali kupunguzia Wakenya gharama ya maisha,” walisema kwenye taarifa yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *