Familia mbili katika eneo la Lumakanda na Malava zimejipata katika njia panda baada yao kukosa kuitambua miili ya wapendwa wao walioaga.
Familia ya marehemu Colleta Vifwafwa Ziezie ilikuwa imeandaa ibaada ya mazishi ya mamayao kabla ya kupokea simu kutoka kwa wahudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti cha kimbilio ambako mwili huo ulikuwa umehifadhiwa wakiombwa kusitisha shughuli za mazishi.
Kulingana na Dillion Mulusa, palikuwa na mchanganyiko wakati wa kuuchukuwa mwili wa mamayao katika makafani na mwili wa mamayao ulikuwa umechukuliwa na familia kutoka eneo la Chegulo karibu na kaunti ndogo ya Malava.
Alisema kuwa familia hiyo ya eneo la Chegulo waliufanyia mwili waliokuwa nao uchunguzi vizuri kabla ya mazishi walipogundua si huo na kumpigia simu mhudumu wa makafani ya Kimbilio.
Aidha familia zote mbili zimekiri kuwa miili hiyo inafanana na ilihitaji kuwa makini Zaidi kabla ya kuitofautisha. “wanafanana sana na kama sio mama mmoja mkongwe kutoka eneo la Chegulo tungezika miili tofauti,” alisema Mulusa.
Ilibidi ibaada kusimamishwa ili familia zibadilishane miili kwa ajili ya maziko.
Tukio hili limewaacha wakaazi vinywa wazi.
“inashangaza kuwa familia zote mbili zilishindwa kutambua miili ya mama zao,” alimalizia Mzee Joram Mutembuli.